Alhamisi 2 Aprili 2026 - 14:03
Taasisi za Kidini na Kiutamaduni za Kimataifa za Iran Zalaani Mashambulizi ya Marekani na Israel Dhidi ya Shule, Vyuo Vikuu, Maeneo ya Ibada na Miundombinu

Hawza/ Taasisi za kidini, kielimu na kiutamaduni za kimataifa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimetoa tamko la kulaani mashambulizi dhidi ya shule, vyuo vikuu, vituo vya ibada, urithi wa kiutamaduni, miundombinu na wananchi wasio na hatia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, taasisi za kidini, kielimu na kiutamaduni za kimataifa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimetoa tamko la kulaani mashambulizi dhidi ya shule, vyuo vikuu, vituo vya ibada, urithi wa kiutamaduni, miundombinu na wananchi wasio na hatia.

Maandishi kamili ya tamko hilo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa, na hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwapa ushindi.
(Suratul Hajj, aya ya 39).

Kwa wanazuoni watukufu, viongozi wa kidini wa dini na madhehebu mbalimbali, maprofesa wa vyuo vikuu, waandishi na wanahabari, wasomi na watu mashuhuri katika siasa, pamoja na watu wote wapenda uhuru duniani!

Tukiwa na mioyo iliyojaa huzuni kubwa na ghadhabu takatifu, sisi tuliotia saini tamko hili, kwa niaba ya taasisi za kidini, kielimu na kiutamaduni za kimataifa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tunatoa hukumu kali kabisa dhidi ya kuendelea kwa uvamizi wa kikatili unaofanywa na ubeberu wa kiburi wa Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni wa kihalifu dhidi ya vituo vya kisayansi, utafiti, kidini na kiutamaduni vya nchi yetu.

Mashambulizi haya ya kinyama na yasiyo na uungwana yalianza kwa kuuawa kwa njia ya kigaidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Imam Shahidi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei (quddisa sirruhu sharif), sambamba na kuuawa kishahidi kundi la makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi, pamoja na shambulizi dhidi ya Shule ya Msingi ya Shajareh Tayyibah katika mji wa Minab, ambapo zaidi ya watoto 175 wasio na hatia na walimu wao waliuawa shahidi. Mashambulizi hayo hadi sasa yamesababisha vifo vya mamia ya watu, wakiwemo viongozi na raia wasiokuwa na uwezo wa kujilinda.

Hadi sasa, uhalifu huu, mauaji ya kigaidi na mauaji ya halaiki yanaendelea, jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu, kanuni za kimataifa, pamoja na kukanyaga misingi ya maadili, tunu za kidini na dhamiri ya kibinadamu.

Adui huyo mhalifu wa Marekani na Israel, ambaye baada ya mwezi mmoja wa mashambulizi yasiyokuwa na mipaka ameshindwa kukabiliana na wapiganaji mashujaa na hajafanikiwa kufikia hata lengo moja kati ya malengo aliyokuwa ametangaza, bali amepata mapigo makali katika medani zote, sasa kwa woga na udhalili anaendelea kuzilenga shule, vyuo vikuu, maeneo ya ibada, urithi wa kiutamaduni, hospitali, vituo vya uzalishaji na usambazaji wa dawa, majengo ya makazi, taasisi za kutoa misaada ya kijamii na miundombinu.

Katika hali hii, ilitarajiwa kuwa nchi za Kiislamu zingesimama upande wa watu waliodhulumiwa mbele ya uhalifu unaofanywa na makafiri wapiganaji dhidi ya nchi ya Kiislamu na kuuawa shahidi kwa Marjaa wa kidini anayefuatwa na mamilioni ya watu. Hata hivyo, kwa masikitiko na huzuni kubwa, jambo hilo halikutokea.

Kwa hiyo, tunatarajia kwamba wanazuoni, viongozi wa kidini, makasisi na wahubiri wa dini na madhehebu mbalimbali, wasomi na viongozi wa kisiasa, viongozi wa vyama, maprofesa wa vyuo vikuu, waandishi, wadau wa sanaa na vyombo vya habari, viongozi na masheikh wa makabila, wanaharakati wa mitandao ya kijamii, na kwa ujumla watu wote wenye moyo wa uhuru, wanaotetea haki na wanaopinga dhuluma duniani, wasikae kimya, bali wasimame kwa ujasiri na kulaani mashambulizi haya ya kikatili na uhalifu huu wa kutisha wa kivita.

Tunawaomba wanasayansi na wasomi wapenda uhuru, wahubiri wenye mwamko, watu wenye majukwaa yenye hadhira kubwa, wanaharakati wa vyombo vya habari na kila mtu anayejali mustakabali wa mwanadamu, wachukue msimamo thabiti na ulio wazi dhidi ya uhalifu unaofanywa na wapanga njama wa Kizayuni na wanaowaunga mkono kupitia mashambulizi ya mabomu dhidi ya vituo vya kisayansi na utafiti, misikiti na makanisa, raia wasio na hatia, miundombinu, na hata urithi wa kiutamaduni pamoja na mabaki ya kale ya kihistoria ya Iran.

Vilevile, tunawaomba waelimisha umma kuhusu nyanja mbalimbali za vita hivi vya dhuluma katika mikutano, matukio na vyombo vya habari, na kusaidia kuweka mazingira yatakayowezesha viongozi wa serikali ya Marekani yenye umwagaji damu na utawala wa Kizayuni unaoua watoto kutambuliwa kuwa wahalifu katika mahakama za kimataifa.

Mwisho, tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aongoze hatua zenu, na aweke juhudi zenu njema katika mizani ya matendo yenu mema, ili sote tushuhudie kushindwa kwa madhalimu wa dunia na ushindi wa haki dhidi ya batili.

Kwa shukrani na heshima.

Waliotia saini tamko hili:

1. Alireza A’rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Elimu za Kidini za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
2. Mohammad Hassan Akhtari, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (as), na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Ashuraa.
3. Mohammad Mahdi Imanipour, Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu.
4. Reza Ramezani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (as).
5. Hamid Shahriari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kuleta Makubaliano baina ya Madhehebu ya Kiislamu.
6. Ali Abbasi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa (saww).
7. Sayyid Abdulfattah Nawab, Mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya Hija na Ziara za Matukufu.
8. Ahmad Wa’ezhi, Mkuu wa Ofisi ya Uenezi wa Kiislamu.

Tarehe: 13 Farvardin 1405
Sawa na: 13 Shawwal 1447 Hijria/  2 Aprili 2026.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha